KONGAMANO LA UTOTO
MTAKATIFU KANDA YA MASHARIKI 13 – 17/6/2013 JIMBONI IFAKARA
Jimbo Katoliki Ifakara lilikuwa
mwenyeji wa Kongamano la mwaka huu la Utoto Mtakatifu Kanda ya
Mashariki ya
Metropolitan ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Kongamano hilo lilifanyika kati ya
tarehe 13 na 17 Juni, 2013 lilihusisha majimbo manane ambayo ni Ifakara,
Mahenge, Morogoro, Dodoma, Kondoa, Tanga, Zanzibar na Jimbo Kuu la Dar es
Salaam.
Jumla ya Watoto 2 512 na walezi
570 walishiriki kongamano hili. Jumla hii ya walezi inajumuisha pia Mapadri na
Watawa Masista. Maaskofu walioshiriki walikuwa ni pamoja na Mwadhama Kardinali
Polycarp Pengo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Wahashamu Maaskofu
Telesphore Mkude wa Morogoro, Agapit Ndorobo wa Mahenge, Eusebius Nzigirwa
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Askofu Mwenyeji Salutaris
Libena. Jimbo mwenyeji liliwakilishwa na jumla ya watoto 875na walezi 89.
Watoto na Walezi kutoka ndani ya Jimbo waliwasili Jimboni tarehe 10 Juni siku
ya jumatatu kwa mazoezi ya pamoja.
Wageni waliwasili tarehe 13 Juni
siku ya jumatano. Watoto na Walezi walilala kwenye mabweni ya shule ya Benignis,
sekondari ya Kilombero na Chuo cha Ufundi cha Mt. Josef. Tarehe 14 Juni, Baba
Askofu Mwenyeji Salutaris Libena alilifungua rasmi kongamano kwa misa Takatifu
iliyofanyika kwenye uwanja wa mpira wa kituo cha Vijana. Tarehe 15 Juni,
Mhashamu Askofu Eusebius Nzigirwa aliongoza Misa Takatifu eneo hilohilo. Kwa
siku mbili yaani tarehe 14 na 15 Juni, watoto na walezi wao walihudhuri semina
mbalimbali zilizoongozwa na Waheshimiwa Mapadri Dr. Lucas Mahogha wa Jimbo la
Mahenge, Achilleus Ndege wa Ifakara na Sr. Grace Shembetu wa Masista wa Upendo
Jimbo la Mahenge. Kwa siku hizi mbili watoto walipata pia muda wa kuonyesha
vipaji vyao kwa kucheza halaiki, ngoma, na michezo mingine mbalimbali.
Kilele cha Kongamanao kilikuwa
tarehe 16 Juni siku ya Jumapili. Siku hiyo watoto waliamka na kupata kifungua
kinywa baadaye kulifanyika Misa Takatifu kwenye uwanja wa michezo wa Kituo cha
Vijana, misa iliongozwa na Mwadhama Polycarp Cardinali Pengo. Baada ya Misa
Watoto na Walezi walifanya maandamano
yaliyoanzia uwanja wa Ibada hadi posta yakaelekea Soko Mjinga na kupinda
kushoto eneo la Mortuary kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mt. Fransis hadi Kituo
cha Nazareti na kumalizia kwenye uwanja wa mpira wa chuo cha Ufundi. Maandamano
hayo yalipokelewa uwanjani hapo na Maaskofu wote waliohudhuria kongamano
wakiongozwa na Mwadahama Kardinali Pengo.
Baada ya mlo wa mchana, saa 10
jioni watoto, walezi na Maaskofu walikusanyika tena kwenye uwanja wa mpira wa
kituo cha vijana kwa kuhitimisha kongamano ambapo kila jimbo lilitoa taarifa za
shughuri zake kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu kongamano la mwaka jana ambalo
lilifanyika Jimboni Dodoma. Pamoja na shughuri nyingine mbalimbali katika
hitimisho hilo, Jimbo la Ifakara lilitoa zawadi rasmi kwa watoto na walezi wa
Jimbo la Zanzibar. Jimbo mwenyeji lilitoa zawadi ya Msalaba na fedha taslimu
shs. Laki tano. Lengo la zawadi hizo lilikuwa kuwapa pole kwa matukio ya
kuvamiwa na kuuwawa na kuumizwa kwa Mapadri wao na kwa misukosuko yote
wanayoipata inayohusu imani yao katoliki kutoka kwa wapinga Kristo wa huko
Zanzibar. Katika hitimisho hilo, Mwenyekiti wa Maaskofu wa Kanda ya Mashariki
Mwadhama Polycarp Cardinali Pengo alitangaza rasmi kuwa Kongamano la Mwaka
kesho 2014 litafanyika Jimboni Kondoa. Tarehe 17 Juni wageni wote waliondoka
kurudi makwao na wote walifika salama. KAULI MBIU YA KONGAMANO LA MWAKA HUU
LILIKUWA MTOTO NA IMANI. Jimbo linapenda kwanza kumshukuru Mwenyeji Mungu kwa
kulibariki na kuliongoza kongamano hata likafanyika na kwisha kwa usalama na
amani. Pia Jimbo linapenda kuwashukuru watu wote walioshiriki kwa katika
maandalizi na wakati wote wa kongamano hata likafikia malengo yake.
Comments
Post a Comment