Padri Louis Adalbert Mdenkeri alikuwa mtoto wa tatu kati ya watoto wanane kwa baba Adalbert Fidelis Mdenkeri na mama Anthonia Kazingoma. Alizaliwa Kwiro tarehe 31 Machi, 1945. Alibatizwa tarehe 01 Aprili, 1945 namba yake ya ubatizo: Kwiro LB 15093. Alipewa kipaimara na Hayati Askofu Mkuu Edgar Maranta tarehe 01 Oktoba, 1955 namba yake ikiwa LN 10026. Alipewa daraja ya Upadri huko Kwiro tarehe 12 Agosti, 1972 na hayati Askofu Adrian Mkoba wa Morogoro.
MAREHEMU PADRE LOUIS MDENKERI |
Elimu:
Hayati Padri Mdenkeli alisoma darasa la i-iv katika shule ya Msingi Kwiro. Baadaye seminari ndogo ya Mt. Fransis sasa inafahamika zaidi kama Kasita Seminari darasa la tano hadi la kumi. Baada ya kumaliza darasa la kumi pale Kasita aliacha seminari na kujiunga na sekondari ya Mt. Joseph – Jimbo Kuu la Dar es Salaam ambayo baadaye ikaja kuitwa Forodhani secondary school. Wakati anasoma St. Joseph sekondari, Hayati Sr. Yasinta aliyekuwa Mkuu wa shule alimshauri wakati huo kijana Louis Mkenkeli kurudi tena seminarini. Alikubali ushauri huo na aliomba kujiunga na Jimbo Kuu la Dar es Salaam chini ya Hayati Askofu Mkuu Edgar Maranta. Alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho kati ya Mwaka 1967 na 1968 kwa masomo ya falsafa. Na kuanzia Mwaka 1969 hadi 1972 alisoma katika seminari Kuu ya Kipalapala Tabora kwa masomo ya Tauhidi/teolojia na kuhitimu Mwaka 1972 na 12 Agosti Mwaka huo alipewa daraja ya upadri.
Vituo vya kazi:
Kwa kuwa yeye alikuwa padri wa Jimbo Kuu la Dar es salaam, mara baada ya upadrisho alirudi Jimboni kwake na kupangiwa kazi. Kituo chake cha kwanza cha kazi kilikuwa Parokia ya Kipatimu na baadaye Parokia ya Mitole ambazo ziko katika Jimbo la Lindi. Baada ya kutumikia chini ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa miaka kadhaa, aliomba kurudi kufanya kazi katika Jimbo lake la nyumbani, yaani Mahenge, hiyo ilikuwa Mwaka 1976. Kwa miaka thelathini na saba ya kulitumia Jimbo la Mahenge na baadaye Ifakara, Padri Mdenkeri alitoa huduma katika parokia mbalimbali kama Paroko na Paroko msaidizi. Alikuwa Paroko wa kwanza Mzalendo katika Parokia za Mlimba na Taweta akizipokea kutoka kwa Ndugu Wakapuchini. Alikuwa pia Paroko Iragua, Paroko Msaidizi Kisawasawa, Biro na kuanzia Mwaka 1996 hadi kifo chake amekuwa msaidizi hapa Ifakara kwa miaka kumi na saba. Akiwa Paroko Msaidizi wa Ifakara alijitoa kweli kweli katika kuwahudumia wagonjwa, wazee na kuadhimisha misa kwa ajili ya marehemu na huduma nyingine za kipadri.
MARADHI HADI KIFO:
Kuanzia tarehe 26 May, 2013 siku ya jumapili, Padri Mdenkeri alianza kujisikia vibaya kiafya. Siku ya jumatano ya tarehe 29 May, 2013 alikwenda hospitali ya Rufaa ya Mt. Fransis na baada ya uchunguzi wa haraka wa afya yake, waganga waliamuru alazwe. Polepole alianza kupata nguvu lakini ghafla hali yake ilianza kushuka kwa kupata tatizo la kushindwa kupumua vizuri. Waganga walishauri apelekwe Dar es Salaam kwa vipimo na matibabu zaidi. Tarehe 11 Juni alisafirishwa kwenda Dar es Salaam na kulazwa katika hospitali ya TMG. Alikwenda huko akiwa hawezi kujimudu mwenyewe lakini baada ya kupewa huduma, alianza kupata nguvu kidogo. Hali yake ilikuwa ya kupanda na kushuka tatizo kubwa likiwa lilelile la shida ya kupumua na baadaye alianza pia kupa shida ya kutapika kila alipokula. Tarehe 25 juni aliamka, kuoga na kula lakini mara baada ya kumaliza kula chakula cha asubuhi, hali yake ilibadilika na pamoja na juhudi za waganga na wauguzi kumsaidia, hawakuweza, hivyo alifariki dunia. Taarifa ya kifo chake ilikuwa ya kushitua na kuhudhunisha sana lakini sote tulilazimika kukubali mapenzi ya Mungu. Na ndivyo tunavyo waomba nyote kukubali mapenzi ya Mungu.
Mwili wa Marehemu Pd. Mdenkeri uliwasili Jimboni Ifakara usiku wa manane wa tarehe 26 juni 2013. Siku ya alhamisi jioni saa 11, mwili wa marehemu uliletwa kanisani kwa wakristo kutoa heshima zao za mwisho na ulibaki ndani ya kanisa usiku kucha hadi asubuhi. Tarehe 28 juni, 2013 siku ya ijumaa, ilifanyika misa ya mazishi iliyoongozwa na Mhasahmu Askofu Salutaris Libena wa Ifakara. Mapadri wengi wa Jimbo la Ifakara, Mahenge na kutoka nje ya Majimbo haya walihudhuria, pia watawa na umati mkubwa wa Walei.
APUMZIKE KWA AMANI, AMINA
Comments
Post a Comment