Sunday, August 16, 2015

HABARI ZA JIMBO -Toleo la Januari - Juni, 2015  1.  SIKU YA MWANAMKE DUNIANI WAWATA WAKUTANA MPANGA
Tarehe 8 Machi ya kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Mwanamke Duniani. Kijimbo, Wanawake wakatoliki maarufu WAWATA waliiadhimisha siku ya Mwanamke Duniani ngazi ya Jimbo katika Tarafa ya Mlimba Parokiani Mpanga. Ilikuwa siku nzuri pale akina mama kutoka parokia mbalimbali walipokutana kwa semina, mafunzo mbalimbali na siku ya kilele Misa Takatifu na michezo. Mgeni rasmi katika kilele hicho alikuwa Mhe. Pd. Bonaventure Mchalange Naibu wa Askofu wa Ifakara. Mahudhurio ya akina mama kadili ya parokia yalikuwa kama inavyoonekana kwenye jedwali.
Na
Parokia
Idadi

Mwendelezo
1
Taweta
16
11
Ifakara
29
2
Mpanga
47
12
Kibaoni
10
3
Mlimba
24
13
Kiberege
2
4
Chita
12
14
Mkula
11
5
Merera
11
15
Msolwa Ujamaa
1
6
Mchombe
21
16
Nyandeo
14
7
Mbingu
26
17
Mofu
0
8
Namwawala
3
18
Lungongole
0
9
Idete
3
19
Kisawasawa
0
10
Mahutanga
2
20
Mang’ula
0
 …….
 ……………………..
……………
21
Kilombero
0
 …….
 ………………………
 …………….
……..
Jumla kuu
232

Katika picha matukio ya siku ya kilele cha siku ya mwanamke kijimbo.
      
    

  1. SR HILTRUDA LYANIHELA ATUTOKA GHAFLA

Ilikuwa taarifa ya ghafla na ya kusikitisha sana pale Mama Mkuu wa Shirika la Masistaa wa Upendo wa Mt. Fransis wa Assis Jimbo la Mahenge alipotutangazia kifo cha Sr. Hiltruda. Sr. Hiltruda alifariki kwa ajali ya kugongwa na pikipiki maarufu “Bodaboda” asubuhi ya jumapili ya tarehe 14 Juni, 2015 eneo la Msimbazi Centre – Dar es Salaam alipokuwa akivuka barabara ya Kawawawa akielekea kanisani kwa misa ya dominika. Msamaria mwema alimwokota Sr. Hiltruda akiwa mahututi na kumkimbiza katika hospitali ya amana – Ilala na baada ya Uongozi wa Shirika kupata taarifa ulikwenda hospitalini na kumhamishia katika hospitali
ya Taifa Muhimbili. Pamoja na juhudi za madtari kuokoa uhai wake, Sr. Hiltruda alifariki dunia majira ya saa 5 asubui. Sr. Hiltruda alizikwa katika makaburi ya Masista Itete tarehe 17 Juni, 2015. Sr. Maria Hiltruda alizaliwa mwaka 1942 Kwiro Mahenge kwa baba Paulo Chigumbi Lyanihela na mama Maria Kamando, amefariki akiwa na umri wa miaka 73. Sr. Hiltruda alitegemewa kuadhimisha jubilei ya miaka 50 ya utawa mwakani, 2016.
APUMZIKE KWA AMANI
 

  1. KWA HERI PADRI DISMAS UBISHIMBALI “STABLE”
 Mtu wa watu, mtani, mcheshi, muwazi, asiye na kinyongo Pd. Dismas Ubishimbali alitoweka ghafla kama utani vile. Ilikuwa asubuhi ya tarehe 30 Mei, 2015 pale Mapadri na Watumishi wa Nyumba ya Mapadri Ifakara walipoingia chumbani mwake alimofikia na kumkuta akiwa amefariki. Pd. Ubishimbali alikuwa amefika Ifakara akitokea Kwiro kwa lengo la kuhudhuria mazishi ya Baba Mdogo wa Padri Filbert Mhasi. Pd. Ubishimbali ambaye alijiita na kutambulika kwa majimba ya utani kama vile “mzungu”, “mzungu mpakistani”, “stable”, nk. Alizaliwa 15/02/1950 kwa baba Clarence Michael Ubishimbali na mama Clara Iddi Antoni Ubaratu. Kwa asili Pd. Ubishimbali ni mzaliwa katika kijiji cha Ebuyu wakati huo ikiwa chini ya Parokia ya Sali Jimbo la Mahenge na familia yake ilihamia Ifakara miaka ya 1964/65. Alisoma Kasita na baadaye Seminari Kuu ya Ntungamo na kumalizia Kipalapala Tabora. Alipata daraja ya ushemasi 29/06/1975 na upadrisho 14/08/1976, madaraja yote aliyapata kwa Askofu Patrick Iteka. Alifariki usiku wa kuamkia 30/05/2015 na kuzikwa Kwiro 02/06/2015. 
APUMZIKE KWA AMANI

  1. SFUCHAS WAOMBOLEZA
Jumuiya ya Chuo Kikuu kishiriki cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Mt. Augustino cha Tanzania tawi la Ifakara ilipatwa na msiba mkubwa wa kufiwa na mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho kijana Samweli Lucas. Kijana Samweli alifariki katika ajali ya barabarani katika Mbuga ya Mikumi tarehe 19 Machi, 2015 baada ya basi alilokuwa akisafilia kuja/kurudi Ifakara baada ya likizo fupi ya wiki mbili kugongana uso kwa uso na lori la mizigo na yeye kufariki hapohapo. Marehemu Sanweli alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa kozi ya uganga/udaktari. Kichuo alikuwa Waziri wa Ulinzi katika Serikali ya Wanafunzi ya chuo na mwanamichezo mzuri. Hayati Samweli aliagwa rasmi na jumuiya wa Chuo na wakati wa Ifakara 23/03/2015 na alikizikwa nyumbani kwao Kibaha 24/03/2015. 
APUMZIKE KWA AMANI
                      
Picha ya Marehemu Samweli wakati wa uhai wake           Baba Askofu wa Ifakara na waombolezaji wengine wakitoa heshima zao za mwisho


  1. HOSTELI KIKWAWILA
Mapadri wa Shirika la Utangazaji wa Habari Njema (Heralds of Good News) wanaosimamia kituo cha Watoto Yatima na Wazee cha Kikwawila wamefungua hosteli yao ya wageni iliyokuwa katika ujenzi kwa miaka mingi. Ujenzi wa hosteli hii ulianza na Pd. Fransis aliyekuwa mwanzilishi wa kituo hicho.  Pamoja na nguvu za Shirika, ujenzi wa hosteli hii umepata pia msaada kutoka kwa Wanashirika la “Association Gocce” wa Italia na Mama Maria Tan wa Singapore. Hosteli hii ilibarikiwa na kufunguliwa na Mhashamu Salutaris Libena Askofu wa Ifakara tarehe 16/05/2015 na tukio hilo kushuhudiwa na wawakilishi wa “Association Gocce” ambao ni Anna, Fabian na Torante anayefanyakazi Chuo cha Manesi cha Edgar Maranta.


  1. ASHEREHEKEA MIAKA 20 YA UASKOFU
Mhashamu Agapiti Ndorobo Askofu wa Jimbo la Mahenge aliadhimisha Jubilei Ndogo ya kutimiza Miaka 20 ya Utumishi katika Jimbo la Mahenge kama Askofu. Sherehe hii ilifanyika tarehe 16/06/2015 kwa misa takatifu iliyoanza kuanzia saa 10 jioni katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme Kwiro na baadaye kufuatiwa na tafrija kubwa na nzuri. Askofu Ndorobo alitangazwa kuwa Askofu wa Mahenge 21/03/1995 na kusimikwa rasmi 16/06/1996. Sisi Wanajimbo la Ifakara tunampongeza sana Baba Askofu kwa kutimiza miaka hii ya utumishi kama Askofu na tunamwombea Baraka za Mwenyezi Mungu apate afya njema na nguvu zaidi za kulitumikia taifa la Mungu.Friday, June 28, 2013

PADRE LOUIS MDENKERI HATUPO NAE TENA

Padri Louis Adalbert Mdenkeri alikuwa mtoto wa tatu kati ya watoto wanane kwa baba Adalbert Fidelis Mdenkeri na mama Anthonia Kazingoma. Alizaliwa Kwiro tarehe 31 Machi, 1945. Alibatizwa tarehe 01 Aprili, 1945 namba yake ya ubatizo: Kwiro LB 15093. Alipewa kipaimara na Hayati Askofu Mkuu Edgar Maranta tarehe 01 Oktoba, 1955 namba yake ikiwa LN 10026. Alipewa daraja ya Upadri huko Kwiro tarehe 12 Agosti, 1972 na hayati Askofu Adrian Mkoba wa Morogoro.
 
MAREHEMU PADRE LOUIS  MDENKERI
 
Elimu:

Hayati Padri Mdenkeli alisoma darasa la i-iv katika shule ya Msingi Kwiro. Baadaye seminari ndogo ya Mt. Fransis sasa inafahamika zaidi kama Kasita Seminari darasa la tano hadi la kumi. Baada ya kumaliza darasa la kumi pale Kasita aliacha seminari na kujiunga na sekondari ya Mt. Joseph – Jimbo Kuu la Dar es Salaam ambayo baadaye ikaja kuitwa Forodhani secondary school. Wakati anasoma St. Joseph sekondari, Hayati Sr. Yasinta aliyekuwa Mkuu wa shule alimshauri wakati huo kijana Louis Mkenkeli kurudi tena seminarini. Alikubali ushauri huo na aliomba kujiunga na Jimbo Kuu la Dar es Salaam chini ya Hayati Askofu Mkuu Edgar Maranta. Alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho kati ya Mwaka 1967 na 1968 kwa masomo ya falsafa.  Na kuanzia Mwaka 1969 hadi 1972 alisoma katika seminari Kuu ya Kipalapala Tabora kwa masomo ya Tauhidi/teolojia na kuhitimu Mwaka 1972 na 12 Agosti Mwaka huo alipewa daraja ya upadri.

 

Vituo vya kazi:

Kwa kuwa yeye alikuwa padri wa Jimbo Kuu la Dar es salaam, mara baada ya upadrisho alirudi Jimboni kwake na kupangiwa kazi. Kituo chake cha kwanza cha kazi kilikuwa Parokia ya Kipatimu na baadaye Parokia ya Mitole ambazo ziko katika Jimbo la Lindi. Baada ya kutumikia chini ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa miaka kadhaa, aliomba kurudi kufanya kazi katika Jimbo lake la nyumbani, yaani Mahenge, hiyo ilikuwa Mwaka 1976. Kwa miaka thelathini na saba ya kulitumia Jimbo la Mahenge na baadaye Ifakara, Padri Mdenkeri alitoa huduma katika parokia mbalimbali kama Paroko na Paroko msaidizi. Alikuwa Paroko wa kwanza Mzalendo katika Parokia za Mlimba na Taweta akizipokea kutoka kwa Ndugu Wakapuchini. Alikuwa pia Paroko Iragua, Paroko Msaidizi Kisawasawa, Biro na kuanzia Mwaka 1996 hadi kifo chake amekuwa msaidizi hapa Ifakara kwa miaka kumi na saba. Akiwa Paroko Msaidizi wa Ifakara alijitoa kweli kweli katika kuwahudumia wagonjwa, wazee na kuadhimisha misa kwa ajili ya marehemu na huduma nyingine za kipadri.

 

MARADHI HADI KIFO:

Kuanzia tarehe 26 May, 2013 siku ya jumapili, Padri Mdenkeri alianza kujisikia vibaya kiafya. Siku ya jumatano ya tarehe 29 May, 2013 alikwenda hospitali ya Rufaa ya Mt. Fransis na baada ya uchunguzi wa haraka wa afya yake, waganga waliamuru alazwe. Polepole alianza kupata nguvu lakini ghafla hali yake ilianza kushuka kwa kupata tatizo la kushindwa kupumua vizuri. Waganga walishauri apelekwe Dar es Salaam kwa vipimo na matibabu zaidi. Tarehe 11 Juni alisafirishwa kwenda Dar es Salaam na kulazwa katika hospitali ya TMG. Alikwenda huko akiwa hawezi kujimudu mwenyewe lakini baada ya kupewa huduma, alianza kupata nguvu kidogo. Hali yake ilikuwa ya kupanda na kushuka tatizo kubwa likiwa lilelile la shida ya kupumua na baadaye alianza pia kupa shida ya kutapika kila alipokula. Tarehe 25 juni aliamka, kuoga na kula lakini mara baada ya kumaliza kula chakula cha asubuhi, hali yake ilibadilika na pamoja na juhudi za waganga na wauguzi kumsaidia, hawakuweza, hivyo alifariki dunia. Taarifa ya kifo chake ilikuwa ya kushitua na kuhudhunisha sana lakini sote tulilazimika kukubali mapenzi ya Mungu. Na ndivyo tunavyo waomba nyote kukubali mapenzi ya Mungu.

Mwili wa Marehemu Pd. Mdenkeri uliwasili Jimboni Ifakara usiku wa manane wa tarehe 26 juni 2013. Siku ya alhamisi jioni saa 11, mwili wa marehemu uliletwa kanisani kwa wakristo kutoa heshima zao za mwisho na ulibaki ndani ya kanisa usiku kucha hadi asubuhi. Tarehe 28 juni, 2013 siku ya ijumaa, ilifanyika misa ya mazishi iliyoongozwa na Mhasahmu Askofu Salutaris Libena wa Ifakara. Mapadri wengi wa Jimbo la Ifakara, Mahenge na kutoka nje ya Majimbo haya walihudhuria, pia watawa na umati mkubwa wa Walei.

APUMZIKE KWA AMANI, AMINA

 
Wednesday, June 26, 2013

WATOTO WA KITUO CHA BETHLEHEM WAPATA AJALI


Watoto wapatao 103, Walezi na Wafanyakazi wa Kituo cha Bethlehem jumla yao yapata kama 160 walipata ajali ya gari siku ya jumanne ya tarehe 25 juni, 2013 majira ya saa 11 jioni wakati wakituri kutoka pikiniki. Ajali hiyo ilitokea eneo la Kijiji cha Kilama B baada ya Fuso lililo wabeba kuingia katika shimo na kuanguka. Kati ya Walezi waliopata ajali alikuwepo pia Sr. Salome. Masista wengine walezi walirudi kwa gai nyingine. Mkurugenzi wa Kituo cha Bethlehem, Padri Basil Ngwega alieleza kuwa Watoto, Walezi na Wafanyakazi wa Kituo cha Bethlehem huwa na kawaida ya kufanya pikiniki wakati wanapofunga likizo la mwaka. Na mara hii walichagua kwenda Kilama B kwa pikiniki. Aliendelea kusema kuwa wakati wakirudi, gari ambalo lilibeba kundi kubwa zaidi lilitumbukia kwenye mtaro na kuegama baadaye kuanguka upande wa kulia mwa gari. Katika ajali hiyo, watoto wapatao 20 na walezi 5 waliweza kupata majeraha mbalimbali. Kati yao watoto 2 waliumia kichwani na kushonwa na walezi 4 walipumzishwa katika hospitali ya Mt. Fransis kwa uchunguzi zaidi. Hadi tunaandika taarifa hii, watoto wote walio pumzishwa wameruhusiwa na kati ya Walezi, ni mmoja tub ado yuko hospitali kwa matobabu.
TUNAWAPA POLE WOTE WALIOFIKWA NA AJALI HII NA KWA WALIOUMIA TUNAWAOMBEA WAPONE HARAKA.